Rais wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Ahmed Yahaya amesema TFF imekuwa ikiingilia utendaji wa bodi hiyo.
Katika mahojiano na moja ya vituo vya redio jijini hapa leo asubuhi, Yahaya, amesema baadhi ya watendaji wakuu wa shirikisho hilo la soka nchini wamekuwa wakiingilia majukumu ya TPLB, jambo ambalo alidai limekuwa wakati mwingine likisababisha mvutano kati ya taasisi hizo mbili.
“Ni kweli TFF imekuwa ikiingilia utendaji wa bodi likiwamo suala hili la ratiba ya ligi kuu. Bodi ya ligi ni chombo cha TFF, kwa hiyo kinalazimika kuitii TFF, lakini wakati mwingine tunakataa kufuata wanachotaka,” Yahaya amesema na kuongeza:
“Wanapofanya uamuzi wenye malengo mazuri ya kujenga, tunakubali. Wanapotaka kufanya mambo ambayo yako kinyume, tunawakatalia kama tulivyowapinga walipotaka tukaguliwe mahesabu yetu (TPLB) na ‘auditor’ (mkaguzi) ambaye hakuidhinishwa na mkutano mkuu wa TFF.
“Tulipata barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa TFF, akitutaarifu kwamba wanatutumia ‘auditor’ kwa ajili ya kupitia mapato na matumizi yetu, tulikataa kwa sababu mkaguzi wa fedha za TFF na vyombo vyake ni lazima aidhinishwe na mkutano mkuu wa wanachama wa TFF.”
Kauli hiyo ya Rais wa TPLB imetolewa ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi kutoa tamko la kuzipiga kalenda mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara za JKT Ruvu Stars dhidi ya Yanga na ya Mgambo JKT dhidi ya Azam FC ambazo bodi ilipanga zichwe leo, Jumatano.
Meneja wa timu ya Azam, Jemedari Said, alisema jana kuwa walilazimika kuahirisha safari yao ya kwenda Tanga jana baada ya kupata barua kutoka kwa Ofisa Mashindano wa TFF, Idd Mshangama, ikiwataarifa kuhusu uamuzi wa Malinzi kuziahirisha mechi za katikati ya juma hili.
“Ilikuwa tusafiri leo (jana) kwenda Tanga, lakini tumepata barua kutoka kwa Mzee Mshangama ikieleza kuwa Rais wa TFF (Malinzi) ameziahirisha mechi zote za ligi kuu zilizopangwa kufanyika Jumatano (leo),” alisema Jemedari.

No comments:
Post a Comment